Alikiba na Diamond ‘Mkizembea’ Aslay na Rayvanny Watawanyamazisha

Kwa sasa ukizungumzia wasanii wa Bongo Fleva wanaofuatiliwa zaidi nchini Tanzania kwenye muziki na maisha yao nje ya muziki, haipingiki kuwa ni Diamond Platnumz na Alikiba.

Kufuatiliwa kwao ni kutokana na wingi wa mashabiki wao na uzuri wa muziki wanaoufanya hiyo ndiyo sababu kubwa inayowafanya kuvuna mashabiki kila uchwao.

Hakuna ubishi kuwa vipaji vyao ni vikubwa na huenda pia muziki wao umewashawishi baadhi ya wasanii kuingia kwenye tasnia hiyo, ila umeshawahi kujiuliza uwepo wa Aslay na Rayvanny kwenye muziki wa Bongo Fleva?

Bila shaka kwa miaka 7 jina la Aslay limekuwa likisika kwenye masikio ya wengi kutokana na kazi zake ingawaje watu wengi mwanzoni walikuwa wanachukulia muziki wake kama unalenga zaidi watoto, inawezekana dhana hiyo ilitokana na umri wake.

Hata hivyo umri ukasogea kidogo Aslay akaingia kwenye kundi la Yamoto Band kundi ambalo lilikuwa linaundwa na wasanii wanne Beka Flavour, Maromboso, Enock Bella na Aslay.

Hakuna ubishi kuwa kundi hili lilikua kwa muda mfupi sana Afrika Mashariki na kutajwa kwenye tuzo nyingi kubwa barani Afrika.

Kutokana na kukua kwa kundi hilo la Yamoto Band jina la Aslay lilikuwa halisikiki kwa sana, hii ilisababisha watu wengi wasione uwezo wake lakini ukweli ni kwamba alikuwa na msaada mkubwa kwenye kundi hilo.

Ukweli kuwa Aslay ana kipaji cha kipekee na uwezo mkubwa wa kutunga na kuimba umekuja kudhihirika mwaka huu mwezi Mei baada ya kundi la Yamoto Band kusambaratika na kila msanii kuanza kufanya kazi kivyake.

Kusambaratika kwa kundi kukaruhusu Aslay kuanza kurudisha makali yake kwa kuanza kufanya kazi kama ‘Solo Artist’ na ukweli ni kwamba tangu aanze kufanya kazi mpaka sasa ni miezi mitano na tayari ameachia ngoma kali saba.

Wimbo wake wa kwanza ulikwa ni Angekuona, Usiitie ndoa doa akiwa na Khadija Kopa, Muhudumu, Baby, Likizo, Pusha na wimbo wake mpya aliouachia jana (Jumatano) Natamba.

Ukweli ni kwamba nyimbo zote hizo tayari zimeshatazamwa na zaidi ya watazamaji milioni 1 kwenye mtandao wa Youtube, na kati ya nyimbo hizo hakuna wimbo ambao haujaingia kwenye Top 10 za Radio na TV hapa nchini.

Hakuna ubishi Aslay nyimbo zake zote akipanda jukwaani anaimba na mashabiki mwanzo mwisho hii ni ishara kuwa muziki wa Aslay unasikilizwa sana nchini na kikubwa ni kwamba ameuacha muziki wake ufanye kazi na sio kwa kiki au kwa maneno maneno ili asikike kwenye media.

Nakumbuka kuna kipindi Beka ambaye walikuwa wote kwenye la Yamoto Band baada ya kumuona Aslay anang’ara kwa kuachia ngoma mfululizo alianza kutoa kauli za kumpinga lakini Aslay hakumjibu hii yote ili kuufanya muziki wake umtambulishe yeye na sio jina lake lijulikane kwa stori tofauti na muziki.

Anachokionesha Aslay kipo sawa pia na anachokifanya Rayvanny kutoka WCB kwani naye ni moja ya vijana ambao nadiriki kusema tunajivunia kuwa nao kwenye muziki wetu wa Bongo Fleva.

Kipaji chake nae pia kilianza kuonekana toka kitambo kwenye mashindano ya Serengeti Fiesta Super Nyota huko mkoani Mbeya.

Licha ya kipaji chake na uwezo wa kutumia vifaa mbalimbali vya muziki, kuimba na kurap kwa pamoja na uwezo mkubwa wa utunzi lakini mafanikio yake yalianza kuonekana mapema alipojiunga na lebo ya WCB ingawaje amekaa muda mrefu chini ya kundi la Tip Top.

Kwa miezi mitano Rayvanny ameachia ngoma nne kali ambazo ni Mbeleko, Chuma ulete, Unaibiwa na Zezeta na nyimbo zote tayari zimetazamwa na watazamaji zaidi ya milioni 1 kwenye mtandao wa Youtube na kufanya vizuri kwenye chati mbalimbali za radio na runinga hapa nchini na kuoneshwa na vituo vikubwa vya runinga barani Afrika.

Rayvanny pia ndani ya mwaka mmoja aliojiunga na WCB amefanikiwa kupata tuzo ya BET na kuwa msanii wa kwanza Tanzania kuchukua tuzo hiyo kubwa duniani.

Rayvanny ameanza kufahamika kwa watu wengi mwaka jana baada ya kuachia ngoma yake ya ‘Kwetu’ na tayari amepata mafanikio makubwa ikiwemo tuzo ya BET ambayo yote hayo yamekuja kutokana na uwezo wake na kuacha muziki wake mzuri umtambulishe zaidi kwa mashabiki kuliko kuzungumziwa kwa kiki/drama kwenye muziki wake.

Kama utakuwa ni mfuatiliaji wa show za Rayvaany utaungana nami kuwa hakuna shabiki asiyeimba naye awapo jukwaani.

Bila shaka wasanii wote hawa wawili ukiwatazama kwa sura ya muziki unaona kabisa safari yao ya muziki inaelekea kuzuri na Watanzania wameshaanza kuwaamini kwa kile wanachokifanya na hakuna ubishi wanaweza watafika mbali.

Kwanini nasema Diamond Platnumz na Alikiba wasibwete hapa walipo?

Kama nilivyosema awali uwezo wa wasanii hawa ni mkubwa na wamepata mafanikio makubwa kwenye muziki ila muziki wao umejaa skendo na hao wameshajijengea mazingira hayo na hawataki muziki wao uende bila kutupiana vijembe mitandaoni au kwenye media.

Ifikie mahala mtambue kuwa hata wasanii wadogo kwa sasa kutokana na nyinyi kuishi maisha hayo, na wao wanapigania kufanya muziki uliojaa na drama ili mradi wajulikane na wapate show. Imefikia muda hata wasanii wanatafuta interview kwenye media sio kuongelea kazi zao ila kutafuta kiki kwa kuwakashifu wasanii wengine.

Ninaposema ‘MKIZEMBEA’ nimemaanisha kuwa endapo mtaendelea kufanya kazi kwa mazoea kwa sababu ya ukubwa wa majina yenu huku mkitupiana vijembe kwenye mitandao ya kijamii na vyombo vya habari, bila shaka wasanii kama Aslay na Rayvanny ambao wapo bize wakikesha kuumiza vichwa kwa kiu ya kuwafikia kimafanikio. Hakuna ubishi safari yao ya kuwafikia itakuwa fupi na watawaacha midomo wazi kama hadidhi ya Mr. Nice na Dudubaya.

Kumbukeni waswahili wanasema hakuna marefu yasiyo na ncha, sasa ili kugeuza huu msemo msiridhike kwa kelele za mashabiki endeleeni kukaza buti na maneno ya mashabiki yabaki kuwa changamoto kwenu.

Jump to original: 

Alikiba na Diamond ‘Mkizembea’ Aslay na Rayvanny Watawanyamazisha