Nassari:Hakuna Dhamira ya Dhati ya Kuchunguza Shambulio la Tundu Lissu

Mbunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Joshua Nassari ameeleza kuwa vyombo vinavyohusika na uchunguzi wa tukio la kushambuliwa kwa risasi Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu havina dhamira ya dhati ya kuufanya uchunguzi huo.

Nassari ameongea hayo kufuatia na kauli ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba kusema kuwa, Tundu Lissu atakuwa msaada mkubwa katika upelelezi wa tukio hilo pale atakaporudi nchini.

“Mtu ameshambuliwa yuko kitandani, hatujui atapona siku gani, hatujui atarudi lini nchini, hatujui atarudi katika hali gani, eti wanamsubiria aje kufanya upelelezi. Akirudi baaada ya miaka miwili?”

“Na huo Upelelezi utakaokuja kufanyika baada ya miaka miwili ni upelelezi wa aina gani!…. Kwa hiyo mimi nafikiri dhamira ya dhati haipo,” alieleza Joshua Nassari.

Alieleza kuwa amesikitishwa na kitendo cha waziri anayesimamia wizara nyeti nchini kusema kuwa, wanamsubiri Tundu Lissu apone ndipo uchunguzi uendelee.

“Waziri huyo huyo amezungumza kwamba wanamsubiri Tundu Lissu apone ili aweze kuwasaidia kufanya upelelezi. Tundu Lissu angekufa maana yake upelelezi usingekaa ufanyike?” alihoji Nassari.

“Nilipomsikia Mwigulu akiongea nikiwa Nairobi, nilisikitika kidogo kwa sababu ni kijana msomi na mtu wa umri mdogo ambae anajua teknolojia zilizopo duniani kwa sasa hivi. Kwa hivyo ni aibu kusema kwamba watafanya upelelezi kwa vyombo vya ndani na wanamsubiri Tundu Lissu apone ndipo aje awasaidie kufanya upelelezi.” aliongeza.

“Angekufa maana yake upelelezi usingefanyika. Kwa maana hiyo watanzania hatuko salama…”

Visit site: 

Nassari:Hakuna Dhamira ya Dhati ya Kuchunguza Shambulio la Tundu Lissu