Makonda Ameondoa Uhalali wa Rais Kusimamia Matendo yake..Chadema Wafunguka

Chama cha Demokrsia na Maendeleo (CHADEMA) kimesema kwamba, Rais Magufuli amepoteza uhalali wa kusimamia kile alichokifanya kipindi cha nyuma baada ya kumtetea kiongozi anayedaiwa kuwa ameghushi vyeti.

Tamko la CHADEMA limekuja ikiwa ni saa chache tangu Rais aliposema kuwa, baadhi ya watu wanasema kuwa Makonda hajasoma, lakini kwake hata kama hajasoma na hajui A lakini anakamata dawa za kulevya, huyo ni msomi mzuri.

“Je! Rais anajua kuwa kauli yake ya leo (jana) kuonesha kuwa ‘vyeti’ si suala muhimu, ameondoa uhalali wowote ule uwe wa kisheria au wa kisiasa wa agizo lake la kuwafukuza watumishi wale waliodaiwa kutokuwa na vyeti?” walihoji CHADEMA katika taarifa yao walioitoa jana.

CHADEMA wamesema kuwa, miezi kadhaa iliyopita kinyume na sheria na taratibu, Rais aliagiza kuondolewa kwenye utumishi wa umma watumishi zaidi ya 9,000 baada ya kudaiwa walikuwa na vyeti vya kughushi, lakini leo anasimimama na kuonyesha kuwa, suala la vyeti si la msingi kama mtu anaweza kufanya kazi.

Aidha, wamehoji kama kweli Rais Magufuli alimaanisha aliposema kwamba serikali yake haitalea vilaza (watu wasio na sifa stahiki) alipokuwa akizungumzia sakata la wanafunzi waliodahiliwa kusoma programu maalum ya ualimu katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).

“Je! Rais Magufuli anajua kuwa kauli yake ya leo (jana) inaonesha kuwa hakuwa na nia ya dhati kupinga ‘vilaza’ kwenye serikali yake? Na kwamba hakuwa mkweli kwa sababu wapo vilaza anaowatetea?

Baada ya madai ya utata wa majina anayotumia Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaama na elimu yake kutopatiwa majibu wala ufafanuzi, Meya wa Manispaa ya Ubungo, Boniface Jacob, alifungua shauri mbele ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, ili mamlaka hiyo ishughulikie suala hilo kwa kadri ya sheria za nchi na kumaliza utata uliopo.

CHADEMA wameeleza kuwa kauli ya Rais Magufuli inaingilia shuari hilo ambalo bado halijapatiwa ufumbuzi na kwamba inaiweka Sekretairieti ya Maadili katika wakati mgumu.

Katika taarifa yao, CHADEMA wameonyesha kushangazwa na kauli ya Rais Magufuli kuwa hajapandisha na wala hatopandisha mishahara ya wafanyakazi kwani bado anayokazi kubwa ya kuwaletea wananchi maendeleo, lakini kwenye sherehe za Mei Mosi, Rais aliahidi kuwa katika bajeti ya 2017/18, kungekuwa na nyongeza ya mishahara ya watumishi.

Hata hivyo, CHADEMA wamemkumbusha Rais kwamba, amekuwa akisema yeye ni mtetezi wa wanyonge, ni vyema akajua kuwa miongoni mwa wanyonge ni pamoja na wafanyakazi hao wanaoomba kuongezewa kima cha chini cha mshahara.

By Swahili Times

Link:

Makonda Ameondoa Uhalali wa Rais Kusimamia Matendo yake..Chadema Wafunguka