Wataalamu Bingwa wa Dawa za Usingizi Afrika Mashariki Wakuta na Dar

Wataalamu Bingwa wa Dawa za Usingizi Afrika Mashariki Wakuta na Dar

Wataalamu bingwa wa dawa za usingizi Afrika Mashariki wamekutana katika Kitengo cha Mifupa (MOI) kwa ajili ya mafunzo ya siku nne yanayotolewa na Chuo Kikuu cha Afya Kwa Zulu Natal kwa kushirikiana na Chama cha madaktari wa Dawa za Usingizi nchini(Sata).

Mafunzo hayo ambayo kwa mara ya kwanza yanafanyika nchini Tanzania, yanaongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ambaye pia ni daktari bingwa wa dawa za usingizi, Mpoki Ulisubisya.

Akizungumza na vyombo vya habari leo Jumanne, Dk Ulisubisya amesema mafunzo hayo yatasaidia uwezo wa madaktari bingwa kushughulikia magonjwa ya ajali kwa watoto.

Amesema mafunzo hayo yametayarishwa na Sata kwa kushirikiana na kampuni ya kuuza dawa za usingizi Abbvie, ili kusaidia madaktari bingwa wa upasuaji kupata uelewa wa ni jinsi gani ya kuhudumia upasuaji wa usingizi.

Amesema kampuni hiyo imekuwa ikitoa misaada mbalimbali kwa upande wa mabingwa wa usingizi nchini na imeweza kupeleka wataalamu kwenda kupewa mafunzo Kwa Zulu Natal nchini Afrika Kusini ambao wana kila kitu cha kujifunzia hivyo kumwezesha mtaalamu kufanya mafunzo kwa vitendo.

“Vifaa au midoli hii ya kufundishia ni salama zaidi ikilinganishwa na kufanya mafunzo kwa vitendo kutumia binadamu, kwani faida ya kutumia hii hata kama ukikosea huwezi kusababisha madhara yoyote kiafya,” amesema Dk Ulisubisya.

Kwa upande wake daktari bingwa wa dawa za usingizi kwa watoto kutoka Hospitali ya Taifa Rwanda, Dk Rosemary Mukunzi amesema mafunzo hayo ni ya kwanza kutolewa Afrika Mashariki lakini yamekuwa yakitolewa Kusini mwa Jangwa la Sahara, “ni mafunzo muhimu kwa wataalamu wa dawa za usingizi kwani ni sekta nyeti na muhimu, hata hivyo duniani wataalamu wake ni wachache.”

Credit:  

Wataalamu Bingwa wa Dawa za Usingizi Afrika Mashariki Wakuta na Dar