Rais Magufuli atoa ahadi kwa viongozi wa serikali za mitaa

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amewataka viongozi wa mamlaka za Serikali za Mitaa kuunga mkono juhudi mbalimbali zinafanywa kutetea rasilimali za taifa, kujenga uchumi na kurekebisha dosari zinazosababisha kero kwa wananchi ili kujenga Tanzania mpya.

Mhe. Rais Magufuli amesema hayo leo wakati akifungua mkutano mkuu wa 33 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa (ALAT) unaofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam na kujumuisha viongozi na watendaji wakuu wa Majiji, Manispaa, Miji na halmashauri za Wilaya.

Mhe. Rais Magufuli ametaja juhudi zilizofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano tangu ilipoingia madarakani miezi 23 iliyopita kuwa ni pamoja na kudhibiti matumizi yasiyo ya lazima na kuongeza ukusanyaji wa mapato ya Serikali kutoka Shilingi Bilioni 850 hadi kufikia Shilingi Trilioni 1.3, kuongeza bajeti ya maendeleo kutoka asilimia 26 hadi kufikia asilimia 40, kutoa elimu ya msingi na sekondari bila malipo kwa kutoka ruzuku ya Shilingi Bilioni 23.868 kila mwezi, kuongeza bajeti katika huduma za afya na kutekeleza miradi ya maji katika miji na vijiji mbalimbali nchini.

Juhudi nyingine ni kuimarisha miundombinu ya usafiri kwa kuanza ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge) kati ya Dar es Salaam na Morogoro na baadaye Morogoro – Dodoma kwa Shilingi Trilioni 7, kununua ndege 6 kwa ajili ya shirika la ndege la taifa, upanuzi wa bandari za Dar es Salaam, Mtwara na Tanga, Ununuzi wa meli mbili za ziwa Nyasa, ujenzi wa viwanja vya ndege, barabara za juu Jijini Dar es Salaam na barabara ya njia 6 ya Dar es Salaam – Chalinze pamoja na kuendeleza mradi wa mabasi yaendayo haraka Jijini Dar es Salaam (BRT).

Mhe. Rais Magufuli ameongeza kuwa Serikali inaendelea na juhudi za kuongeza uzalishaji wa umeme kutoka megawatts 1,460 zinazolishwa hivi sasa hadi kufikia megawatts 5,000 ifikapo mwaka 2020 kwa kujenga miradi ya uzalishaji umeme kwa kutumia gesi na kujenga mradi wa umeme katika maporomoko ya mto Rufiji (Stieglers’ Gorge), kuongeza vijiji 7,873 vitakavyopata umeme na hivyo kufikia vijiji zaidi ya 12,259 ifikapo mwaka 2021, kusimamia biashara ya madini kwa manufaa ya Watanzania, kusimamia ipasavyo usambazaji wa pembejeo na kujenga mazingira bora ya uwekezaji.

Mhe. Rais Magufuli amewahakikishia viongozi hao kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imejipanga kufanya juhudi kubwa zaidi zenye manufaa kwa nchi na hivyo ametoa wito kwa viongozi hao kutoa ufafanuzi wa dhamira hiyo kwa wananchi na kushirikiana kutekeleza mipango na miradi kwa kutanguliza maslahi ya taifa.

“Nataka niwaambie ndugu zangu adui yetu sio vyama vya siasa, adui yetu ni wanaotuibia rasilimali zetu, hivyo twende pamoja, tushirikiane kuijenga nchi yetu” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli na kuwataka viongozi hao kuondoa tofauti na migogoro iliyopo kwenye mamlaka zao.

Aidha, Mhe. Rais Magufuli amewapongeza viongozi hao kwa kazi kubwa wanayoifanya  kusimamia utekelezaji wa miradi mbalimbali na mipango ya Serikali na amewahakikishia kuwa changamoto zinazowakabiri zitafanyiwa kazi ili kuongeza ufanisi wa mamlaka hizo.

Mkutano huo umehudhuriwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa pamoja wadau mbalimbali wa maendeleo wa halmashauri kutoka taasisi na mataifa mbalimbali.

Gerson Msigwa

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

03 Oktoba, 2017

Dar es Salaam

More here – 

Rais Magufuli atoa ahadi kwa viongozi wa serikali za mitaa