Mtoto Aliyefungiwa Chumbani kwa Miezi Sita Aanza Matibabu

Mtoto Aliyefungiwa Chumbani kwa Miezi Sita Aanza Matibabu

Mtoto Mariam John (12), mkazi wa Nyamongo wilayani hapa aliyekuwa amefungiwa ndani kwa zaidi ya miezi sita, ameanza kupata matibabu baada ya kuokolewa, huku mzazi wake akijitetea kuwa uwezo wa kumhudumia ndio uliochangia.

Mariam aliokolewa na Kituo cha Kutetea Haki za Binadamu cha Masanga kilichopo wilayani hapa baada ya wazazi kumfungia ndani kutokana na ugonjwa wa degedege huku akiwa na tatizo la akili.

Mzazi wa mtoto huyo, Paulina John alisema kuwa mwanaye alianza kuugua ugonjwa huo tangu Januari 2017 na kuvimba mwili wote, na wakati huo mama huyo alikuwa na mtoto mwingine aliyekuwa anaumwa hivyo alishindwa kuwahudumia wote kwa pamoja.

Kamanda wa Polisi Tarime/Rorya, Henry Mwaibambe alisema wanamshikilia mama huyo huku akiendelea kumhudumia mwanaye hadi atakapopata nafuu ndipo atakapofunguliwa mashtaka ya kumficha na kumnyima chakula.

Hata hivyo, kamanda huyo alisema baba wa mtoto huyo alikimbia kusikojulikana kukwepa mkono wa sheria, lakini wanamsaka ili naye ajibu tuhuma hizo.

Mkurugenzi wa Kituo cha Haki za Binadamu Masanga ambacho pia kinatoa huduma za afya, Stella Mgaya alisema kwa sasa mtoto huyo ameanza kuonyesha matumaini ya kuimarika kiafya.

Msimamizi wa kituo hicho, Julius Joshua alisema mtoto huyo alipokewa kituoni hapo Septemba 26 akiwa na hali mbaya na hakuwa na uwezo wa kukaa wala kuona vizuri kutokana na kudhoofika mwili na alipopimwa aligundulika kuwa na utapiamlo uliopitiliza.

“Tulipompima uzito siku hiyo alikutwa na kilo 12, lakini baada ya kukaa hapa kituoni kwa siku chache amepimwa na kukutwa amefikisha kilo 16, hilo ni jambo la kufurahisha,” alisema Joshua.

Alisema walipata taarifa za mtoto huyo kutoka kwa majirani kwamba amefungiwa ndani.

Meneja wa kituo hicho, Valerian Mgani alisema baada ya mtoto huyo kufikishwa walimwanzishia chakula lishe ili kumpa nguvu na kuujenga mwili ambapo kwa sasa mtoto huyo anaweza kukaa na kuona vizuri.

See the original post:  

Mtoto Aliyefungiwa Chumbani kwa Miezi Sita Aanza Matibabu