Video: Ushahidi wa Nassari jinsi Madiwani wa CHADEMA Arusha walivyonunuliwa

Mbunge wa Arumeru Mashariki (CHADEMA), Joshua Nassari ameweka hadharani ushahidi wa rushwa waliopewa madiwani wa chama hicho ambao wamejiuzulu kwa nyakati tofauti na kujiunga Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa kile walichosema kuwa ni kumuunga mkono Rais Dkt Magufuli.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumapili Oktoba Mosi, Mbunge Joshua Nassari aliyekuwa ameambatana na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless  Lema alitoa ushahidi huo wa video na kusema kwamba ataukabidhi kwa Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Valentino Mlowola.

Katika mkanda wa video alioucheza Mbunge Nassari, sauti mbalimbali zilisikika ambapo imeelezwa kuwa miongoni mwazo ni ya Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Alexander Mnyeti na Mkurugenzi wa Halmashuri ya Meru, Christopher Kazeri wakiwaahidi madiwani hao mambo mbalimbali ikiwamo kuwapatia posho zao za vikao vilivyosalia hadi 2020.

Mbali na hilo, imeelezwa kuwa Madiwani hao walitaka pia wapewe fedha na kupatiwa ajira pamoja na kukamilishwa miradi yote ya maendeleo waliyoahidi kwa wananchi wakati wa uchaguzi.

Aidha, katika video hiyo, diwani mmoja amesikia akiomba kugharamiwa gharama za kufunga harusi huku wengine wakiahidiwa kupewa makazi mapya.

Nassari amesema kuwa ametumia miezi kadhaa kukusanya ushahidi huo na ameutoa sasa kwa sababu umekamilika. Aidha, amesema kwamba alitumia vifaa vya kisasa kutoka nchini Uingereza alimokuwa akisoma, katika kukusanya ushahidi huo.

Licha ya wabunge hao kuweka hadharani ushahidi huo, Madiwani hao waliwahi kunukuliwa mara kadhaa wakisema kuwa hawakujiuzulu kwa sababu ya fedha, bali walifurahishwa na utendaji kazi wa Rais Dkt Magufuli na hivyo kuamua kumuunga mkono.

More here:  

Video: Ushahidi wa Nassari jinsi Madiwani wa CHADEMA Arusha walivyonunuliwa